08 February 2012

Muhimbili yafungwa

*Huduma zote zasitishwa hadi kitakapoeleweka
*Tamko la serikali lasubiriwa kuokoa jahazi
*Wizara yahaa kutafuta madaktari wa ziada
Na Waandishi Wetu
Vitanda vya wagonjwa vikiwa tupu kufuatia mgomo wa madaktari na wauguzi unaoendela katika Hospitari ya Taifa ya Muhimbili (MNH), madaktari bingwa na wauguzi wa hospitari hiyo wameungana katika mgomo huo kuanzia juzi, Dar es Salaam jana. (Picha na Michael Machellah)


HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MHN) imetangaza rasmi kusitisha utoaji wa tiba baada ya kuathiriwa na mgomo hadi hapo Serikali itakapotoa tamko rasmi kuhusu muafaka wake na madaktari.
Uamuzi wa hospitali hiyo kubwa kuliko zote nchini kusitisha kutoa huduma ulitangazwa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa MNH Bw. Aminieli Aligaesha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema huduma hizo zimesitishwa kuanzia juzi kutokana na  kamati ya madaktari bingwa kuandikia uongozi kwa MNH,Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Tiba (MUHAS) kusitisha utoaji wa huduma zote zinazotolewa na hospitali hiyo.

Kwa msingi huo alisema huduma zitaendelea baada ya muafaka kupatikana.

Alisema kuwa wagonjwa walioko wodini wataendelea kuonwa na madaktari wachache waliojitolea, na wakuu wa idara  waliopo hospitali hapo, ambapo madaktari wa JWTZ wataendelea kuona wagonjwa wa dharura.

Alisema kwa takwimu walizonazo kuanzi usiku wa juzi na jana asubuhi wapo wagonjwa 811 waliolazwa wodini na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Hata hivyo alisema hali hospitalini hairidhisi kutokana na huduma kuendelea kudorora kila wodi, huku vitengo vingine vikiwa hakuna huduma hata moja inayoendelea.

Waandishi wa habari walipotembelea jengo la watoto walibaini hakuna huduma zozote  zinazoendelea katika wodi hizo.

Akizungumza katika wodi hiyo Bi. Adela Shomari alisema kuwa tangu afike hospitali hapo mtoto wake hajapatiwa matibabu kwani licha ya kuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji.

"Tangu nifike hospitali hapo kutoka Shinyanga mtoto wangu hajapatiwa matibabu zaidi ya kupewa vidonge vya kuongeza damu na panado," alisema.

Naye Saida Kassimu ambaye anamuuguza mtoto anayeumwa ugonjwa wa ngozi alianza kutokwa machozi baada ya waandishi wa habari kufika kwenye kitanda chake na kuanza kusimulia hali iliyopo hospitalini hapo.

"Roho inaniuma, nalia kwa uchungu nikiona mwanangu akiteseka, sina amani kwani leo ni siku ya tano tangu nilipofika hospitali hapo sijawahi kuonwa na daktari," alisema.

Habari ambazo gazeti hili lilipata ni kuwa Waziri wa Afya na ustawi wa jamii,Dkt. Haji Mponda,Naibu waziri Dkt. Lucy Nkya, Katibu Mkuu Bi Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Bw. Deogratasia Mtasiwa, jana usiku walitembelea hospitali hiyo  saa sita usiku wa kuamkia jama ili kujionea hali ilivyo.

Wakati huo huo viongozi wa Wizara ya Afya na  Ustawi wa Jamii, kutwa nzima ya jana walishinda wakihaha kwa lengo la kutafuta madaktari wa kupeleka Muhimbili ili kuokoa jahazi.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana Ofisa Habari, Bw. Nsachris Mwamwaja alisema jana walikuwa wakitafuta madaktari wa kwenda kutoa huduma kwa baadhi ya wodi.

"Juzi kilikaa kikao na kuchukulia suala hilo kama dharura, hivyo iliamuliwa wachukuliwe madaktari wa wizara na kupelekwa Muhimbili," alisema na kuongeza;

"Jana tumehangaika huku na kule kutafuta madaktari hao, lakini hadi muda huu sina uhakika wamepatikana wangapi."

Alisema madaktari hao si mbadala wa tatizo, lakini watakuwa wanatoa msaada kwa zile kazi zilizopo hospitali hapo ambazo zimeachwa kabisa wakati ufumbuzi wa mgogoro huo ukiendelea.

"Sasa hivi tupo tunahangaika ili kuona ni jinsi gani tunaweza kupunguza idadi ya vifo," alisema. Wakati hayo yakiendelea suala hilo liliibuka bungeni jana mjini Dodoma baada ya Mbunge Godfrey Dhambi, kuomba mwongozo kwa Spika Bi Anna Makinda, akitaka kusitishwa kwa kikao cha bunge ili kujadili mstakabari wa madaktari.

Lakini mwongozo huo ulipingwa na Spika Makinda kwa maelezo kuwa suala hilo lipo katika kamati maalumu, hivyo ni vema kusubiri majibu kutoka kwa kamati hiyo.

Kutokana na kusitishwa lwa huduma katika hospitali hiyo, baadhi ya wadau wamesema ni lazima serikali itambue kuwa wananchi wanapoteza maisha, hivyo suala hilo linahitaji ufumbuzi wa haraka.

Mtanzania aliyeishi Ufaransa, Bw. Mohamed alisema  Serikali imeshindwa kuonesha utu kwa kushindwa kumaliza suala hilo.

"Hili ni tatizo kubwa na hasa inapofikia hata kiongozi mkuu akashindwa kusema jambo lolote," alisema Bw. Mohamed .

Alisema viongozi wengi ni wabinafsi ndiyo maana wameshindwa kuchukua uamuzi mapema.

Naye Bw. Bw.Edgar Mwankuga alisema serikali imeshindwa kuweka maslahi ya wananchi mbele hasa katika huduma za muhimu kama sekta ya afya.

"Rais kuendelea kukaa kimya kuhusu mgogoro huo ni ishara tosha kuwa hana uchungu na sisi wananchi ambao kipato chetu hakituruhusu kwenda kutibiwa nje ya nchi",alisema Bw.Mwankuga

Naye Bi.Julieth Swai mkazi wa Dar es Salaam alisema watendaji wa JK wameshindwa kusuruhisha mgogoro huo kwa sababu kila kukicha hali inakuwa mbaya hasa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

2 comments:

  1. Ikifungwa kwao viongozi ni heri,maana wao wanatibiwa india na private hospt.muhimbili,temeke na za mikoa wanakuwepo wakesha hoi wasio na uwezo wa private,tukubali kwa hilo.viongozi wetu hawana uchungu na nyie wa muhimbili,mbona tangu mgomo hawajafika pale,kaenda tu mbatia.jamani wala haviwachomi,wanasubiria mipango ya posho wajipange kutanua na familia zao.taifa linakwisha.

    ReplyDelete
  2. Tusiwalaumu sana viongozi wetu kwani huenda wamefikia kikomo cha uwezo wao kutatua matatizo yetu, hili likiwa ni moja wapo! wangekua wanajua la kufanya wangeisha fanya!

    Watanzania wenye jibu la tatizo hili hawapo kwenye safu ya uongozi wamesogezwa pembeni na mfumo wetu dhalimu.

    Wenye mawazo ya kumaliza tatizo hili amkeni mseme kwani najua mpo huko Tanzania, mpo tele!

    ReplyDelete