07 February 2012

Wanafunzi 11,968 wafaulu la saba kidato II, Zanzibar

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

JUMLA ya wanafunzi 11,968, wamefaulu elimu ya msingi na sekondari katika mitihani waliofanya mwaka jana, visiwani Zanzibar.

Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Ramadhan Abdallah Shaaban, alisema kati ya wanafunzi 11,041 waliofaulu mtihani wa kidato cha pili kuingia cha tatu, wasichana  6,066, wavulana 4,975.

Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 56.1 ya wanafunzi 19,666 waliofanya mitihani wa kidatu cha pili katika shule mbalimbali visiwani humo.

Bw. Shaaban alisema, wanafunzi 927 wamefaulu mtihani wa darasa la saba ambapo kati ya hao, 84 wamefaulu kujiunga na shule za vipaji maalumu.

Kati ya wanafunzi hao, 56 wanatoka Unguja na 28 kutoka Pemba ambapo wanafunzi 843, wamechaguliwa kujiunga na sekondari mbalimbali zilizopo visiwani humo.

Alisema wanafunzi 22, wamefutiwa matokeo baada ya kufanya udanganyifu katika mitihani yao.


Alisema kesi za udanganyifu ambazo zimebainika katika mtihani huo mwaka 2011 zipo 17, kati ya hizo, 12 zinahusisha shule zilizopo Unguja na tano zilizopo Pemba.

“Wanafunzi wote 22, tumewafutia matokeo baada ya kubaini wamehusika na udanganyifu wa aina mbalimbali, kesi 12 ni za mtihani wa kidato cha pili, tano za darasa la saba”, alisema.

Alizitaja shule ambazo wanafunzi wake wamefutiwa matokeo na idadi ya wanafunzi katika mabano kwa Mkoa wa Mjini Magharibi kuwa ni  Jang’ombe Sekondari (1), Mwembeladu Sekondari (2) na Kidongo Chekundu Sekondari (2).

Mkoa wa Kusini ni Mtende Sekondari (1) na Kikungwi (1), Mkoa wa Kaskazini Pemba ni Kangagani (3) na Ole Sekondari (01), Kusini Unguja ni Miwaleni (3), Kiongoni (2), Kajengwa (2) na Kitogani (01), Mkoa wa Kaskazini Pemba Minugwini (1) na Mkoa wa Kusini Pemba, Kisiwa Panza (1).

No comments:

Post a Comment